a

WAHUUMIWA KWENDA JELA KWA KOSA LA USHOGA

Mahakama moja nchini Misri imewahukumu watu wanne kifungo cha hadi miaka minane jela kwa kosa la vitendo vya kufanya mapenzi ya jinsia moja.
Watu hao wanashutumiwa kuhudhuria au kupanga tafrija za vitendo vya ngono, na kuvaa mavazi ya kike na kujipodoa.
Sheria ya Misri haitamki kupiga marufu vitendo vya mapenzi ya jinsia moja, lakini waendesha mashitaka wametumia sheria ya Misri inayokataza mambo fulani kufanyika hadharani kuwahukumu wapenzi wa jinsia moja.
Hukumu hiyo imeshutumiwa na wanaharakati wa haki za binadamu.
misri
Mmoja wa watu hao amehukumiwa na mahakama mjini Cairo, kifungo cha miaka mitatu jela na kazi ngumu.
Kikundi cha kutetea haki za binadamu chenye makao yake nchini Marekani, Human Rights First , kimesema hukumu hizo zinasikitisha na kukatisha tamaa.
“Misri ni taifa linalobadilika katika eneo la nchi za Kiarabu; kinachotokea Misri kinaweka hali ya kuenea katika ulimwengu wote wa nchi za Kiarabu,” kimesema kikundi hicho katika taarifa yake.
Kikundi hicho kimesema tangu kung’olewa madarakani Rais Mohammed Morsi mwezi Julai 2013 kumekuwa na ongezeko la watu kukamatwa kwa misingi ya jinsia zao.
Hukumu ya sasa inakumbushia kesi ya mwaka 2001 ya watu 52 kushutumiwa kwa vitendo vya mapenzi ya jinsia moja na makosa mengine chini ya sheria ya Misri.
Watu ishirini na watatu walihukumiwa kifungo cha kufikia miaka mitano jela pamoja na kazi ngumu, hukumu ambayo ilishutumiwa kimataifa.
Kikundi kimoja cha kutetea haki za binadamu nchini Misri kimesema adhabu kali zilizotolewa kwa watu hao Jumatatu ni sehemu ya msako unaoendelea dhidi ya uhuru binafsi.
Previous
Next Post »