a

Yanga yaandaa sherehe

Yanga yaandaa sherehe

Wachezaji wa Yanga wakishangilia bao katika moja ya mechi katika uwanja wa Taifa.

YANGA leo ina matumaini makubwa ya kutangaza ubingwa katika mechi ya Ligi Kuu itakayochezwa kwenye uwanja wa Taifa Dar es Salaam dhidi ya Polisi Morogoro.
Yanga inahitaji pointi tatu kutwaa ubingwa huo kwani itafikisha pointi 55 ambazo hazitafikiwa na timu yoyote. Azam inayoshika nafasi ya pili ikiwa na pointi 45 itafikisha pointi 54 endapo itashinda mechi zake tatu zilizosalia.
Ingawa kwenye mpira lolote linaweza kutokea, lakini kwa mwenendo wa matokeo inayopata Yanga katika mechi zilizopita, ni wazi Polisi ina kazi kubwa kuizuia leo.
Yanga iliifunga Ruvu Shooting mabao 5-0 katika mechi iliyopita wakati Polisi ililazimishwa sare ya bila kufungana na Coastal Union. Katibu Mkuu wa Yanga Dk Jonas Tiboroha alisema jana kuwa uongozi tayari umeanza maandalizi kusherehekea ubingwa kwa mtindo wa aina yake.
“Uongozi wa Yanga unapenda kuwaalika wanachi wa Tanzania na nchi jirani kuungana nasi kesho (leo) katika shamra shamra za ushindi wa ubingwa wa michuano ya Ligi Kuu nchini,” ilisomeka sehemu ya taarifa ya Dk Tiboroha kwa waandishi wa habari.
“Sisi kama Yanga tumejipanga kwa staili ya tofauti kabisa katika kuuchukua ubingwa wa Ligi Kuu,” alisema. Akizungumzia mechi ya leo kocha wa timu hiyo, Hans van der Pluijm alisema anatarajia kufika safari ya ubingwa salama leo.
“Tuna matumaini makubwa ya kuibuka na ushindi katika mchezo wa kesho (leo) na huo ndio tunaotegemea kutangaza ubingwa,” alisema.
Alisema si kwamba atapata ushindi kirahisi bali amewaandaa wachezaji wake vizuri na anaamini watafanya alivyowaelekeza ili kuibukia na ushindi na kutangaza ubingwa mapema.
Yanga watasafiri kwenye Tunisia kucheza mechi ya marudiano ya Kombe la Shirikisho na Etoile de Sahel ya huko itakayochezwa mwishoni mwa wiki hii

 

Previous
Next Post »