a

Serikali yatangaza ajira za walimu 30,000

Serikali yatangaza ajira za walimu 30,000

 

 

 

Dar es Salaam. Serikali imetangaza ajira mpya za walimu 31,056 wanaotakiwa kuanza kazi kuanzia Mei Mosi, mwaka huu.
Mbali na walimu, pia imetangaza ajira kwa mafundi sanifu wa maabara 10,625 ambao pia wataanza kazi sambamba na walimu hao.
Akizungumza jana, Katibu Mkuu Ofisi ya Waziri Mkuu, Tawala za Mikoa na Serikali za Mitaa (Tamisemi), Jumanne Sagini alisema Serikali imetenga Sh9 bilioni kwa ajili ya posho za kujikimu na nauli kwa walimu na mafundi sanifu maabara.
Alisema kiasi cha fedha kilichotengwa ni posho ya siku saba na fedha za nauli ambazo zinatakiwa kulipwa na halmashauri ambazo ndiyo mwajiri.
Alisema posho hizo zinatakiwa kulipwa ndani ya siku saba na kwamba isizidi siku 14 tangu kuripoti kwa mwalimu katika kituo cha kazi.
“Hatutapenda kusikia malalamiko kutoka kwa walimu hao, halmashauri zijipange kuwapokea waajiriwa wao wapya,” alisema.
Mwaka jana kulikuwa na malalamiko ya baadhi ya walimu wapya ambao licha ya kuripoti kwenye vituo vya kazi, walicheleweshewa posho za kujikimu na nauli.
Alisema idadi hiyo ya watakaoajiriwa inajumuisha walimu 11,795 wa ngazi ya cheti, 6,596 wa stashahada na 12,666 wa shahada.
Alisema walimu 2,700 wa masomo ya sayansi na hisabati wamepangwa moja kwa moja kwenye shule ambazo hazina walimu wa masomo hayo.
“Tofauti na walimu hawa wa sayansi waliopangiwa moja kwa moja kwenye shule zisizo na walimu, walimu wa masomo ya sanaa, kilimo, michezo na elimu maalumu watapangiwa vituo vya kazi na halmashauri,” alisema.
“Walimu wa masomo ya sayansi na hisabati ni wachache ndiyo maana tumeamua kuwapangia moja kwa moja kwenye vituo ili kuhakikisha kila shule inakuwa na walimu wa hisabati baiolojia, fizikia na kemia,” alisema.
Sagini alisema ajira za walimu kwa mwaka huu zimeelekezwa zaidi katika halmashauri zenye uhaba mkubwa wa walimu ili kuweka uwiano sawa na bora wa mwalimu na mwanafunzi kitaifa.(source;mwananchi.co.tz)

Previous
Next Post »