a

Yanga kupewa kombe Mei

Yanga kupewa kombe lake Mei 6


Mashabiki wa timu ya soka ya Yanga wakishangilia baada ya timu yao kutwaa ubingwa wa Ligi Kuu Tanzania Bara baada ya kuifunga Polisi Moro kwa mabao 4-1 katika mchezo uliofanyika kwenye Uwanja wa Taifa juzi. (Picha na Yusuf Badi) 
MABINGWA wapya wa soka Tanzania Bara, Yanga watakabidhiwa kombe lao la ubingwa wa Ligi Kuu katika mchezo kati yao na Azam FC utakaochezwa kwenye Uwanja wa Taifa, Dar es Salaam, Mei 6, mwaka huu.
Kwa mujibu wa taarifa ya Shirikisho la Soka Tanzania (TFF) jana kwa vyombo vya habari, Waziri wa Habari, Vijana Utamuduni na Michezo, Dk Fennela Mkangara anatarajiwa kuwa mgeni rasmi katika sherehe za kukabidhi kombe hilo.
Yanga ilitwaa taji la msimu huu wa 2014-2015 juzi baada ya kuicharaza Polisi Morogoro mabao 4-1 na kufikisha pointi 55 ambazo haziwezi kufikiwa na timu nyingine 13 zinazoshiriki ligi hiyo iliyoanza Septemba 20, mwaka jana.
Kwa ubingwa huo, Rais wa TFF, Jamal Malinzi ametuma salamu za pongezi kwa Mwenyekiti wa Klabu ya Young Africans, Yusuf Manji kutokana na timu yake kutwaa ubingwa wa Ligi Kuu msimu wa 2014/2015.
Katika salamu zake za pongezi, Malinzi amesema Yanga kutwaa ubingwa ni jambo muhimu na sasa wanapaswa kuanza maaandalizi kwa ajili ya michuano ya kimataifa barani Afrika mwakani.
Katika hatua nyingine, baada ya kuiongoza Yanga kutwaa ubingwa huo, Kocha Mkuu Hans van der Pluijm amesema ni rekodi nzuri ya kujivunia kwake na wachezaji wake, lakini hawapaswi kubweteka.
Pluijm alisema wana kazi kubwa ya kuhakikisha wanatinga hatua ya makundi ya michuano ya Kombe la Shirikisho Afrika dhidi ya Etoile Sportive du Sahel ambayo katika mchezo wa kwanza wa hatua ya 16 bora walitoka sare ya bao 1-1 kwenye Uwanja wa Taifa, Dar es Salaam.
“Tunafurahi kutwaa ubingwa nahii inatokana na kazi kubwa tuliyoifanya msimu huu, lakini hatupaswi kuridhika na ubingwa wa nyumbani bado tuna kazi kubwa ya kufanya kuhakikisha tunakwenda Tunisia kupata ushindi dhidi ya Etoile ili tucheze hatua ya makundi,” alisema Pluijm.
Mholanzi huyo alisema ubingwa umewapa ari ya kufanya vizuri kwenye mechi ya marudiano itakayopigwa Mei Mosi mjini Sousse, na imani hiyo inakuja baada ya kuwasoma vizuri wapinzani wao wiki moja na nusu iliyopita.
“Tunakwenda Tunisia nikiwa najivunia ari na hamasa waliyokuwa nayo wachezaji…naamini katika mchezo wa marudiano watacheza kwa nguvu na kuwabana wapinzani wetu ili tuweze kupata ushindi na kusonga mbele japo naamini mchezo utakuwa mgumu,” alisema Pluijm.(source:habarileo.co.tz)
Previous
Next Post »